Tuesday, August 27, 2013

Ufafanuzi kuhusu wafadhili kujitoa kufadhili shughuli za UKIMWI Tanzania

Dk. Mrisho (aliyeketi) akibadilishana mawazo na akina mama walio katika mapambano dhidi ya UKIMWI na VVU huko Kisarawe hivi karibuni
Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) – Tanzania imepata taarifa kutoka kwenye vyombo  vya habari kwamba wahisani wa shughuli za UKIMWI kujitoa kufadhili shughuli za UKIMWI kuanzia mwaka kesho 2014.
 
Maafisa wa Tume
Sehemu ya wanafunzi wa Minaki High School ambao wamejipanga kupambana na maambukizi ya VVU wakiwa shuleni kwao
TACAIDS, inafafanua kwamba tetesi hizo sio za kweli hata hivyo baadhi ya Wahisani ambao wanajitoa kwenye ufadhili kutokana na miradi wanayoifadhili kuisha muda wake au kubadilika vipaumbele kwa mfano Serikali ya Kanada na Denmark ambao wamekuwa  wakisaidia Programu za UKIMWI kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Jamii ambapo mradi wao unaisha 2016/17. Hata hivyo Serikali ya Denmark bado ina nia ya  kuendelea kusaidia shughuli za UKIMWI, baada ya Mradi  huo kuisha.

Utekelezaji wa shughuli za UKIMWI Tanzania umekuwa ukipata ufadhili wa fedha kutoka Serikali ya Tanzania na Serikali za Nchi Marafiki. Programu zinazotekelezwa hufuata Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NMSF).Mpaka sasa kuna uhakika wa fedha za UKIMWI kwa miaka mitano (5) ijayo.

Serikali za nchi Marafiki wamekuwa wakisaidia shughuli za UKIMWI kwa mtindo wa Miradi (Projects) ambayo ni ya muda mfupi kama vile miaka mitatu (3) mpaka mitano (5).  Kwa kawaida miradi huisha na mingine huanza kila mwaka. 

Kwa sasa hivi miradi mingi inatekelezwa kwa kipindi cha Maisha ya Mkakati wa nchi wa UKIMWI ambao unaisha mwaka wa fedha 2017/18.  Wahisani wakubwa wa shughuli za UKIMWI ni Serikali ya Marekani na Mfuko wa Dunia wa Magonjwa ya UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria. 

Wahisani hawa wawili wanatoa kiasi cha 80% ya fedha za UKIMWI nchini na ndio wanaofadhili Programu ya Tiba ya UKIMWI nchini na Programu zao bado zinaendelea na hawajatangaza kujitoa.

Baada ya Miaka 30 ya shughuli za UKIMWI, Tanzania sasa hivi inafahamu maambukizi ya VVU makubwa yanapatikana katika maeneo gani ya Jamii.  Mfano; Makundi ya Wanandoa, Wauza ngono, Wanaofanya ngono ya jinsia moja, Wanaotumia dawa za kulevya na Maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto. 

Hivyo mikakati mingi sasa hivi inaelekezwa katika maeneo hayo ikiwamo kuongeza Tiba kwa WAVIU ambao wanapata tiba vizuri inakuwa ni kinga kubwa hata kwa wenzi wao.

Serikali ya Tanzania baada ya kupata uzoefu wa miaka yote hii inaelekeza nguvu kwenye maeneo ambayo yataleta matokeo makubwa na mazuri zaidi ili kufanikisha haya, Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Mfuko wa UKIMWI Tanzania (AIDS TRUST FUND).  Mfuko ambao utachangiwa na Serikali, Wadau wengine nchini pamoja na Wadau wa Maendeleo. 

Mfuko huu unakadiriwa kupunguza utegemezi wa Wahisani kwa 50%. Mfuko huu unategemewa kuanza Mwaka wa Fedha 2014/2015.


Imetolewa na:     
            Mwenyekiti Mtendaji
            Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS)
            Sokoine Drive/Luthuli Street,
            P. O. Box 76987
            Dar es Salaam.
            Tel: +255 22 2122651/2122427,
            Fax: +255 22 2125651,
            Email: ec@tacaids.go.tz
            Website: www.tacaids.go.tz

0 comments:

Post a Comment