Sunday, August 18, 2013

PWANI yataka takwimu sahihi za UKIMWI huku ikionya wapika takwimu

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi Mahiza akiongea na ujumbe wa TACAIDS pamoja na watendaji wake kuhusu masuala ya UKIMWI na VVU


Mwenyekiti Mtendaji wa TACAIDS Dk.Fatma Mrisho akimsikiliza kwa makini mkuu wa Mkoa wakati wa
ziara ya tume mkoani Pwani wiki iliyopita
Wajumbe wa TACAIDS wakiagwa na Kaimu Mganga wa Mkoa Dk.Beatrice Byalugaba
MKUU wa mkoa wa PWANI Bi Mwantuma Mahiza ameitaka Tume ya kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Shirika la Takwimu la taifa (NBS) vifanye hima ili kupata takwimu sahihi za maambukizi ya VVU ili kuusadia mkoa kuweka vipaumbele sahihi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo
“Ni kweli ugonjwa huu unaendelea kuwa tishio mkoani kwetu, lakini tunachanganyikiwa namna ya kuweka vipaumbele kwa kukosa usahihi wa takwimu za maambukizi ya VVU,” Bi Mahiza aliuambia ujumbe wa TACAIDS uliotembelea ofisini kwake juzi ukiongozwa na mwenyekiti Mtendaji wa tume Dk.Fatma Mrisho
Bi Mahiza akaendelea: Hebu shirikianeni na NBS ili mpate takwimu sahihi za UKIMWI mkoani kwetu…maana siku hizi tunabahatisha.
Hata hivyo, hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete amezindua ripoti mpya ya matokeo muhimu ya utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI na malaria nchini. Utafiti huo ulifanyika kati ya mwaka 2011 na 2012 (THMIS).
Kwa mujibu wa Bi Mahiza, kuna  wajanja wengi wenye asasi zisizo za kiserikali (NGOs) ambao  wanatumia uwepo wa barabara kuu ya Morogoro na vituo vya mizani kuupakazia mkoa wetu kuwa eti maambukizi yanatisha kuliko uhalisia wenyewe. Wanafanya hivyo ili kujipatia hela na misaada kutoka kwa wafadhili wa nje wasiojua ukweli wa mambo na uhalisia wenyewe.
Kwa mfano, Bi Mahiza akaongeza, hivi majuzi tu, kuna kijana wa NGO moja mkoani hapa (siitaji jina), alitoa takwimu eti mkoani Pwani kila siku watu 100 huambukizwa VVU. Haa?! nilishangaa sana. Kwa kuwa na mimi nilikuwa mshiriki katika mkutano huo, nilisimama na kumpinga pale pale.
Huo ni uongo usio kuwa na mfano. Kama  ni kweli, si mkoa mzima wenye watu wasiozidi milioni 1 na laki mbili utakuwa umeambukizwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu?. Ina maana sasa hata mimi mkuu wa mkoa tayari nimeshaambukizwa, akahoji kwa masikitiko.
Kama mkuu wa mkoa, sipendi tabia hii ya kupika takwimu iendelee kwani inakwamisha harakati na mipango yetu dhidi ya UKIMWI
Hata hivyo kiongozi huyo alikiri kuwa kuna baadhi ya maeneo mkoani humo maambukizi ya VVU yalikuwa yanazidi kupanda wakati mengine yalikuwa yanashuka. Alitoa sababu za hali hiyo kuwa ni pamoja na uchumi  katika baaadhi ya familia kuwa mdogo na hulka ya mtu binafsi.
Bado watu wetu wanahitaji elimu kuhusu UKIMWI. Msibweteke na elimu mliyoita mwanzoni. Watu wanapaswa kupewa elimu ya ujasiri katika kupima VVU, elimu ya kuwahudumia wagon jwa, elimu ya kujikinga na maambukizi na elimu ya masula ya lishe na VVU—kusema ukweli bado inahitajika hapa, aliongeza Bi Mahiza
Kwa mujibu wa THMIS 2011-2012, asilimia 5.9 ya wanawake na wanaume kati ya miaka 15 na 49 wana maambukizi ya VVU mkoani Pwani . Hii ni zaidi ya asilimia 0.2 ya kiwango cha maambukizi ya kitaifa (5.7%)
Aidha, kiwango cha maambukizi ya VVU ni kikubwa zaidi maeneo ya mijini kwa wanawake na wanaume kuliko maeneo ya vijijini.
Naye kaimu mganga wa Mkoa Dk. Beatrice Byalugaba alibainisha kuwa baadhi ya wakazi wa Dar es salaam na mikoa mingine jirani wamekuwa wakifuata huduma za tiba za VVU (ARVS) mkoani hapo kwa kuogopa kujulikana mkoani kwao ili kukwepa unyanyapaa.
“Utashangaa wagonjwa wengine wakitoka Dar es salaam kuja kufuata huduma hapa kwetu. Ukiwauliza, wanasema wanaogopa kujulikana makwao,” alisema Dk. Byalugaba akisisitiza ukweli wa kwamba huenda mkoa huo unaonekana kuathirika zaidi kutokana na hali hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tume Dk. Mrisho alitoa wito kwa mkoa kuanza kufikiria jinsi ya kuchangia katika harakati dhidi ya UKIMWI pasipo utegemezi wa wafadhili.
“Ni janga jipya la kitaifa jipya ikiwa hatutakuwa na mbinu zetu wenyewe za kulipia huduma za mapambano dhidi ya UKIMWI. Ni ukweli usiofichika tena kuwa wafadili wanazidi kujitoa na huenda mwakani hali ikawa mbaya zaidi,” alisema Dk. Mrisho aliyekuwa amefuatana katika ziara hiyo na mkuu wa kitengo cha sheria Bi Elizabeth Kaganda
Halmashauri zote nchini zimekuwa zikipata mgao wa fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbai kupitia TACAIDS mara mbili kwa mwaka ili kutoa huduma mbalimbali za masuala ya UKIMWI. Lakini, kutokana na kujitoa kwa wafadahili, halmashauri hizo zitapaswa kujichangisha zenyewe ili huduma zilizokwisha anzishwa ziendelee, “la sivyohili  litakuwa janga jipya la kitaifa,” alibainisha Dk Mrisho

0 comments:

Post a Comment