Sunday, February 10, 2013

TONDOKENI TUKAPIME TUNAZIDI KUCHELEWA



  1. Asalamu naitoa kwa wakubwa shikamoni
Mimi ninamengi sana yale niliyobaini,
UKIMWI gonjwa hatari tambueni  asilani,
Tondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.

  1. Naanza kwa dada zangu leo nawaambieni,
Kupima kujua afya ni vema ndugu zanguni
Acheni vaa vimini nakupita mitaani,
Tondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.

  1. Nakuja kwa ndugu zangu wa kiume uwanjani,
Tuacheni ngono zembe zatutia matatani,
Pamoja na wanafunzi waliopo mashuleni,
Tondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.
  1.  Baba na mama zanguni  naomba nisikieni,
Hata Babu pia bibi naomba zingatieni,
UKIMWI hauchagui Fatuma au Shabani,
Tuondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.
  1. Tusiwe nazo tamaa mimi nasema jamani,
Tutapatwa na maradhi UKIMWI nambari wani,
 Mtakuja kukumbuka niliyosema zamani,
Tondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.
  1. Tusifanye ngono zembe hili tulitambueni,
Tusokote ncha kali tukiwa matembezini
Vyachangia mambukizi ya UKIMWI asilani,
Tondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.
  1. UKIMWI hauna dawa gonjwa hili gonjwa gani,
Lazima tujihadhari sisi wote majumbani,
Labda tutanusurika na gonjwa hili jamani,
Tuondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.
  1. UKIMWI umeenea mimi nasema yakini,
Haujulishi kwa macho wewe ukaubaini,
UKIMWI sasa tishio tunaisha majumbani,
Tondokeni tukapime tunazidi kuchelewa.

Mtunzi: Maulidi  A. Ugama
Jina la kisanii: Ujinga si mzigo.
Ikwiriri sanaa group, Rufiji.