Thursday, June 26, 2014

Kampeni ya Linda Goli Lako yaanza Tanzania

Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa Tanzania (YUNA) kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa hivi karibuni wametangaza kuanza kwa kampeni ya “Linda Goli Lako” nchini Tanzania.
“Linda Goli lako” ni mpango wa kimataifa unaosimamiwa na Mradi wa Pamoja wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kushughulikia UKIMWI (UNAIDS) wa kuongeza uhamasishaji kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) duniani kote kwa kupitia michezo na sekta ya muziki.

Vijana kutoka mashirika ya UN walioshiriki katika kampeni hiyo. (kushoto-kulia) ni: Dk Yeronimo Mlawa (UNAIDS), Usiah Nkhoma (UNIC), Sawiche Wamunza (UNFPA) na kiongozi wa YUNA Tanzania (jina halikupatikana)
Kampeni ina lengo la kuongeza ufahamu wa VVU na kuhamasisha vijana kujikita katika Kuzuia Maambukizi ya VVU (Matumizi ya kondomu, upimaji virusi vya Ukimwi kwa hiari, na kupunguza
idadi ya wapenzi).
Nchini Tanzania, kampeni hii inajulikana kwa Kiswahili kama ‘’Linda Goli Lako, kavukavu nomaa’’ kampeni hii ilianza kabla ya kombe la dunia 2014 na itaendelea baada ya kumalizika kwa fainali za kombe hilo.
Lengo ni kuwafikia vijana mbalimbali kwa ujumbe tofauti wa VVU na Mpango Kabambe wa Afya ya Uzazi (SRH) kupitia michezo na vyombo vya habari.
Uhamasishaji wa kampeni hiyo hususan suala la mabadiliko ya tabia zitahusisha, pamoja na mambo mengine, matumizi ya mitandao ya kijamii, michezo hususan mchezo wa mpira wa miguu kama fursa ya kutoa ujumbe na kukuza uelewa wa vijana kuhusu masuala ya afya ya uzazi. Watoa huduma za afya ya uzazi pia watahamasishwa kupitia washirika mbalimbali ili kutoa huduma wakati wowote ambapo vijana watakusanyika kwa ajili ya shughuli za michezo.
Katika wiki ya kampeni kulikuwa na mfululizo wa shughuli za kampeni katika kuhitimisha uzinduzi rasmi wa kampeni ikiwamo vipindi vya redio na televisheni.
YUNA kwa kushirikiana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Cha Diplomasia (CFR) na Chuo Cha Biashara (CBE) walifanya mashindano ya siku mbili ya kandanda Kabla ya Kombe
la Dunia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Hosteli za Mabibo siku ya Jumamosi Juni 7 na Jumapili 8 Juni, 2014 kwa vyuo vikuu vilivyopo Dar es Salaam.
Mgeni rasimi katika uzinduzi huo alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Linus Mgaya. Ujumbe wa kampeni kwa vijana ulizingatia matumizi ya kondomu kama kinga ya mambo mawili, kuzuia maambukizi ya VVU na kwa ajili ya kupambana na mimba zisizotarajiwa miongoni mwa wanafunzi wa Chuo Kikuu; ukikolezwa na ujumbe Linda Goli Lako, Kavu Kavu Nomaaa.
Wakati wa Michezo, huduma za upimaji virusi vya ukimwi kwa hiyari na huduma za Afya ya Uzazi kwa ujumla zitatolewa uwanjani hapo bure.

0 comments:

Post a Comment