Wednesday, December 12, 2012

Madereva wa malori ya mizigo kupima VVU wakiwa safarini


MADEREVA wa malori ya mizigo ya kwenda mikoani na nchi jirani sasa watakuwa hawana shida ya kupata maarifa, elimu na hudumu mbali mbali za Virusi vya UKIMWI—ikiwa ni pamoja na kupima kwa hiari ili kujua hali zao—kutokana na ufunguzi wa kituo cha maarifa ya udhibiti wa ugonjwa huo jana katika eneo la Mdaula, nje kidogo ya mji wa Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Dk.Mrisho akikata utepe wa kuzindua kituo cha Mdaula
Uzinduzi huo uliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dk. Fatma Mrisho na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mh. Ahmed Kipozi pamoja na viongozi mbalimbali wa wilaya na vijiji vya Mdaula, Matuli na Mbena.

Huduma zitakazotolewa na kituo hicho ambacho kimejengwa kwa gharama ya Sh. 57 milioni ikiwa ni mchango wa Mradi wa Kudhibiti UKIMWI Eneo la Maziwa Makuu (GLIA) kupitia TACAIDS pamoja na mchango wa wanajamii wa Mdaula na Halmashauri ya Bagamoyo kwa kutoa wataalam wakati wa ujenzi, ni pamoja na ushauri nasaha na upimaji wa VVU.

Nyingine ni kutoa elimu na maarifa mbalimbali za UKIMWI, burudani kwa jamii kama vile luninga, michezo ya darts na pool pamoja na huduma za intaneti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mrisho alisema uzinduzi huo ulikuwa unabainisha nia ya serikali ya kuleta huduma za jamii ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na vita dhidi ya UKIMWI karibu na wananchi. 

“Nia ya serikali ni kuhakikisha huduma zinafika karibu na kaya. Kwa mfano, wananchi hawapaswi kuendelea kwenda mbali kufuata huduma za tiba, matunzo, upimaji au elimu kuhusu UKIMWI. Badala yake huduma hizi ndizo ziwafuate ili kuwapunguzia mzigo wa safari na usumbufu. Na hiki ndicho kimefanyika hapa siku ya leo,” alisema Dk. Mrisho 

Akasema, pamoja na kuwa kituo hicho kimejengwa ili kuwapa uwepesi madereva wa malori na magari makubwa ya mizigo yaendayo mikoani na nchi ya jirani kuweza kupata huduma mbali mbali na maarifa ya jinsi ya kupambana na VVU pamoja na UKIMWI, wakazi wa Mdaula pamoja na vijiji jirani nao pia watanufaika na kituo hicho.
Jengo la kituo cha maarifa kuhusu UKIMWI, Mdaula

“Mbali na ndugu zetu madereva, ni matumaini yangu pia kuwa kituo hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa vijana na wanawake kujipatia maarifa na elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU—hii itakuwa ni mchango katika kutimiza ndoto yetu ya kutokuwa na vifo, maambukizi mapya wala unyanyapaa vinavyotokana na UKIMWI tena ifikapo mwaka 2015,”

“Kwenu akina mama, ukikutana na m-baba anakwambia anakutaka ki mapenzi, muulize kwanza, umetahiriwa?, kabla hajajibu muulize tena, una kondomu??,” akaongea Dk. Mrisho na kusababisha hadhira nzima kuripuka kwa kicheko

Eneo la Mdaula pamoja na Chalinze ni mojawapo ya vituo maarufu mkoani Pwani ambapo madereva wa magari makubwa na malori ya mizigo hupumzika ili kujipatia mahitaji mbali mbali kabla ya kuendelea na safari. 

Takwimu zilizotolewa jana na Mratibu wa Mkoa wa Tume Dk. Hafidh Ameir zinaonyesha kuwa maambukizi ya VVU katika maeneo hayo ni kati ya asilimia 9 hadi 15 (9% hadi 15%).

Aidha, imebainishwa kwamba visababishi vikuu vya maambukizo miongoni mwa jamii hiyo na nyinginezo hapa nchini ni  kuwa na wapenzi wengi kwa wakati mmoja (MCP); matumizi madogo ya kinga (kondomu) wakati wa kujamiana pamoja na kiwango kidogo cha wanaume wanaotahiriwa.

Kwa mujibu wa Bw. Renatus Kihongo, Mratibu wa Programu za Kanda za Afrika na Kimataifa wa TACAIDS, mradi wa Kudhibiti GLIA ulianzishwa mwaka 1998 kwa ufadhili wa Mashirika ya Kimataifa ya USAID, DFID, UNAIDS na UNHCR. 
Mratibu wa kituo hicho Bi.Beata akitoa maelezo kwa wageni

Madhumuni makubwa ya kuanzishwa kwake ni kupunguza maambukizi ya UKIMWI na athari zake kijamii na kiuchumi katika Eneo la Maziwa Makuu. Nchi hizo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Makao yake makuu ya Jijini Kigali nchini Rwanda.

Utekelezaji wake unafanywa kwa kushughulikia maeneo ambayo huchangia jitihada na mikakati ya Serikali za nchi  wanachama  katika kushughulikia masuala mtambuka ya UKIMWI. Kwa kipindi cha miaka minne mradi huu ulikuwa unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ukishughulikia maeneo  

Mgeni Rasmi Dk.Fatma Mrisho akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa kituo cha maarifa kuhusu UKIMWI, Mdaula. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mh.Ahmed Kipozi
Katika hatua nyingine, shirika la Family Health International (FHI360) limeahidi kukisaidia kituo hicho ili kiweze kutoa huduma endelevu kwa walengwa.

Ahadi hiyo ilitolewa na mwakilishi wa FHI360 katika hafla hiyo Bw. Charles Fungo ambaye shirika lake linaendesha mradi mwingine ujulikanao kama ROADS na ambao umejikita katika kuwafikia watu walio katika maeneo hatarishi ya kuambukizwa VVU mfano wanawake wanaofanya biashara ya ngono na madereva

0 comments:

Post a Comment