Tuesday, August 27, 2013

Ufafanuzi kuhusu wafadhili kujitoa kufadhili shughuli za UKIMWI Tanzania

Dk. Mrisho (aliyeketi) akibadilishana mawazo na akina mama walio katika mapambano dhidi ya UKIMWI na VVU huko Kisarawe hivi karibuni
Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) – Tanzania imepata taarifa kutoka kwenye vyombo  vya habari kwamba wahisani wa shughuli za UKIMWI kujitoa kufadhili shughuli za UKIMWI kuanzia mwaka kesho 2014.
 
Maafisa wa Tume
Sehemu ya wanafunzi wa Minaki High School ambao wamejipanga kupambana na maambukizi ya VVU wakiwa shuleni kwao
TACAIDS, inafafanua kwamba tetesi hizo sio za kweli hata hivyo baadhi ya Wahisani ambao wanajitoa kwenye ufadhili kutokana na miradi wanayoifadhili kuisha muda wake au kubadilika vipaumbele kwa mfano Serikali ya Kanada na Denmark ambao wamekuwa  wakisaidia Programu za UKIMWI kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Jamii ambapo mradi wao unaisha 2016/17. Hata hivyo Serikali ya Denmark bado ina nia ya  kuendelea kusaidia shughuli za UKIMWI, baada ya Mradi  huo kuisha.

Utekelezaji wa shughuli za UKIMWI Tanzania umekuwa ukipata ufadhili wa fedha kutoka Serikali ya Tanzania na Serikali za Nchi Marafiki. Programu zinazotekelezwa hufuata Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NMSF).Mpaka sasa kuna uhakika wa fedha za UKIMWI kwa miaka mitano (5) ijayo.

Serikali za nchi Marafiki wamekuwa wakisaidia shughuli za UKIMWI kwa mtindo wa Miradi (Projects) ambayo ni ya muda mfupi kama vile miaka mitatu (3) mpaka mitano (5).  Kwa kawaida miradi huisha na mingine huanza kila mwaka. 

Kwa sasa hivi miradi mingi inatekelezwa kwa kipindi cha Maisha ya Mkakati wa nchi wa UKIMWI ambao unaisha mwaka wa fedha 2017/18.  Wahisani wakubwa wa shughuli za UKIMWI ni Serikali ya Marekani na Mfuko wa Dunia wa Magonjwa ya UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria. 

Wahisani hawa wawili wanatoa kiasi cha 80% ya fedha za UKIMWI nchini na ndio wanaofadhili Programu ya Tiba ya UKIMWI nchini na Programu zao bado zinaendelea na hawajatangaza kujitoa.

Baada ya Miaka 30 ya shughuli za UKIMWI, Tanzania sasa hivi inafahamu maambukizi ya VVU makubwa yanapatikana katika maeneo gani ya Jamii.  Mfano; Makundi ya Wanandoa, Wauza ngono, Wanaofanya ngono ya jinsia moja, Wanaotumia dawa za kulevya na Maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto. 

Hivyo mikakati mingi sasa hivi inaelekezwa katika maeneo hayo ikiwamo kuongeza Tiba kwa WAVIU ambao wanapata tiba vizuri inakuwa ni kinga kubwa hata kwa wenzi wao.

Serikali ya Tanzania baada ya kupata uzoefu wa miaka yote hii inaelekeza nguvu kwenye maeneo ambayo yataleta matokeo makubwa na mazuri zaidi ili kufanikisha haya, Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Mfuko wa UKIMWI Tanzania (AIDS TRUST FUND).  Mfuko ambao utachangiwa na Serikali, Wadau wengine nchini pamoja na Wadau wa Maendeleo. 

Mfuko huu unakadiriwa kupunguza utegemezi wa Wahisani kwa 50%. Mfuko huu unategemewa kuanza Mwaka wa Fedha 2014/2015.


Imetolewa na:     
            Mwenyekiti Mtendaji
            Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS)
            Sokoine Drive/Luthuli Street,
            P. O. Box 76987
            Dar es Salaam.
            Tel: +255 22 2122651/2122427,
            Fax: +255 22 2125651,
            Email: ec@tacaids.go.tz
            Website: www.tacaids.go.tz

Friday, August 23, 2013

AIDS fight in Tanzania under siege as donors pull out

Dr Mrisho in a group photo with the Kisarawe Community in the fight against HIV and AIDS
Minaki High School students when hosted TACAIDS officials last week
TANZANIA is likely to experience a serious retardation motion in the fight against HIV and AIDS should a vividly pull out of long time donors in the war against the pandemic not get prompt local-based replacement.
The warning was sounded over the weekend by the Executive Chairperson of the Tanzania Commision for AIDS (TACAIDS) Dr Fatma Mrisho when she paid a courtesy call to the Pwani Regional Commissioner, Ms Mwantumu Mahiza.
Dr Mrisho revealed, “ As we are talking now, I have just met the representatives from CIDA and DANIDA—both of whom have confirmed to me that they will no longer contribute to the National Multi-sectroral Strategic Framework (NMSF)—coming the year 2015,”
This translates into that, we as nation; need to get a prompt replacement of the funding, failure of which, all the achievements we recorded in the fight against HIV and AIDS for more than 20 years will experience a heavy blow, remarked Dr Mrisho
The Danish and Canadian Governments through their international support funds, DANIDA and CIDA respectively, make a group of other bilateral donors who have been contributing tirelessly to the NMSF for many years.
Speaking at Kibaha Township, Dr Mrisho called on all the District councils to start mobilizing own funds to address the looming threat of donors pull out
She said, while TACAIDS and other local players were currently working hard to see to it that the long awaited AIDS Trust Fund (ATF) become operational, local councils should start raising funds from their own sources to attend to the already established HIV/AIDS related interventions
The NMSF is the strategy designed by the government through TACAIDS for addressing HIV and AIDS interventions in the regional councils all-over the country.
Some of the interventions are the provision of life prolonging drugs for people living with HIV (ARVs), care and support for people affected or affected by HIV, home-based care for HIV positive people and care of HIV-orphaned kids.
Likewise, another key donor—the US President Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR)—which has been at a fore hand to support anti-AIDS interventions in the country is slowly reducing its support. According to PEPFAR, AIDS is no longer an emergency case; hence, local efforts can easily handle the issue in sustaining the already established infrastructures.
According to TACAIDS Consolidated Budget Recurrent & Development- 2010/2013, Tanzania received a total of about 575 million USD per year for HIV and AIDS national programme.
Funds received in the country were contributed as follows: donor support 98% and Government 2 % of the national programme. 5% contribution by Government includes donors who supports through General Budget Support.
The Government captures funds for HIV and AIDS according to the modality of funding, as most of the funds by donors are coming into the country through direct project implementation only 28% of the funds are captured in the Government books.
The major supporters of HIV and AIDS National response are the US Government (PEPFAR) 72%, and the Global Fund 20%, NMSF Grant from CIDA and DANIDA 4%, and the UN Family 2%

Monday, August 19, 2013

Bagamoyo yaanza kujifadhili vita dhidi ya UKIMWI,VVU

Bi Albina, CHAC wa Bagamoyo akitoa taarifa ya hali ya UKIMWI wilayani humo kwa wajumbe wa TACAIDS waliotembelea Mkoa wa Pwani juzi
Kamishna wa TACAIDS Dk.Rose Mwaipopo akitoa majumuisho ya ziara ya tume Wilayani Bagamoyo. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Bagamoyo Bw. Erasto Mfugale na kulia kabisa ni RCT wa Pwani Dk.Ameir
Wana-kikundi cha UWAMABA--kikundi cha watu waishio na VVU wilayani Bagamoyo na moja ya vikundi vilivyofanikiwa katika kampeni dhidi ya UKIMWI--wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa TACAIDS
HUKU ufadhili katika masuala ya huduma za UKIMWI nchini ukielekea ukingoni, Halmashauri ya Bagamoyo sasa imetangaza kutenga shilingi milioni 25 kuanzia msimu wa 2013-2014 kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI na virusi vya UKIMWI (VVU) wilayani hapo.

Hayo yamebainishwa juzi na Mratibu wa UKIMWI-Pwani (CHAC) Bi Albina Mtumbuka alipokutana na ujumbe wa tume ya kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) uliotembelea ofisini kwake katika ziara iliyolenga kujua hali ya UKIMWI na vichocheo vyake katika mkoa wa PWANI.

Ujumbe wa TACAIDS uliongozwa na Kamshna wa Tume hiyo Dr Rose Mwaipopo.

“Tumeamua kutenga kiasi hicho (shilling mil.25) kuanzia mwaka huu wa fedha ili kuepusha balaa linaloweza kutokea kutokana na kujitoa kwa wafadhili ambao wamekuwa wakitusaidia tangu tulipoanza vita dhidi ya UKIMWI,:” akasema Bi Mtumbuka

Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya zilizo athirika na maambukizi ya VVU nchini.  Kwa mujibu wa matokeo muhimu ya utafiti wa viashiria vya VVU-UKIMWI na Malaria (THMIS 2011-2012), maambukizi ya VVU yalikuwa yamefikia asilimia 6.9

Kwa mujibu wa Bi Mtumbuka, endapo wilaya haitachukua hatua madhubuti, ni wazi kuwa mafanikio yaliyokuwa yamefikiwa katika kutoa huduma mbalimbali za vita dhidi ya UKIMWI yatakuwa hatarini.

“Hatuna jinsi, kujitoa kwa wafadhili wetu kuwe changamoto kwetu ya kujua namna ya kuendeleza mapambano haya, “ akaongeza Bi Mtumbuka.

Taarifa zilizomfikia mwandishi wetu ni kwamba wafadhili ambao wamekuwa wakitoa pesa kwa ajili ya mfuko wa mwitikio wa UKIMWI katika wilaya zote nchini kupitia TACAIDS (NMSF) wametangaza kusitisha ufadhili wao kuanzia mwaka kesho (2014).

Baadhi ya wafadhili hao ni kutoka mataifa ya Canada (CIDA) na Denmark (DANIDA). “Hali itakuwa ngumu katika halmshauri zetu mara jamaa watakapojiondoa rasmi mwaka kesho—hatutakuwa na jinsi zaidi ya kila wilaya kuanza kujichangisha ili mafaniko tuliyoyafikia dhidi ya UKIMWI yasiwe kazi bure, kilisema chanzo chetu.

Kama hakutakuwa na hatua madhubuti za kila wilaya kutafuta vyanzo vingine vya fedha za kukabiliana na UKIMWI, huduma kama vile matibabu kwa wanaoishi na VVU (ARVs), huduma za UKIMWI majumbani, upimaji wa VVU na huduma kwa watoto yatima vyote vitakuwa katika hatari ya kusambaratika, akabainisha Bi Mtumbuka wakati wa majumuisho yake

Katika miezi ya hivi karibuni, TACAIDS na wadau wengine wake wamekua wakihaha kuharakisha uundwaji wa mfuko wa UKIMWI nchini (AIDS Trust Fund). Tume inaamini kuwe uundwaji wa mfuko huo utasitisha utegemezi wa wafadhili katika masuala ya UKIMWI.

“Ni kweli kabisa, kama mfuko huo utapitishwe na bunge, ni dhahiri tutakuwa katika mazingira mazuri kuendeleza kampeni zetu. Hatutakuwa na haja ya kubabaika kama ilivyo sasa,:” alisema Dk. Hafidhy Ameir, Mratibu wa TACAIDS mkoani Pwani

Kuhusu hali ya maambukizi ya VVU Bagamoyo, takwimu za watu waliojitokeza kupima kwa hiari zinaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Desemba 2012 jumla ya watu 19,126 walishauriwa na kupima VVU. Kati ya hao wanaume ni 5,804 na wanawake ni 13,322.

Ukiwa ni mmoja wa miji mikongwe na ya kitalii nchini, Bagamoyo imeathirika zaidi na maambukizi ya VVU kutokana na kuwa na watu wengi wenye tabia na kutoka maeneo tofauti hali inayopelekea kuwa na miingiliano holela ya wa ki-ngono zembe.

Sunday, August 18, 2013

PWANI yataka takwimu sahihi za UKIMWI huku ikionya wapika takwimu

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi Mahiza akiongea na ujumbe wa TACAIDS pamoja na watendaji wake kuhusu masuala ya UKIMWI na VVU


Mwenyekiti Mtendaji wa TACAIDS Dk.Fatma Mrisho akimsikiliza kwa makini mkuu wa Mkoa wakati wa
ziara ya tume mkoani Pwani wiki iliyopita
Wajumbe wa TACAIDS wakiagwa na Kaimu Mganga wa Mkoa Dk.Beatrice Byalugaba
MKUU wa mkoa wa PWANI Bi Mwantuma Mahiza ameitaka Tume ya kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Shirika la Takwimu la taifa (NBS) vifanye hima ili kupata takwimu sahihi za maambukizi ya VVU ili kuusadia mkoa kuweka vipaumbele sahihi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo
“Ni kweli ugonjwa huu unaendelea kuwa tishio mkoani kwetu, lakini tunachanganyikiwa namna ya kuweka vipaumbele kwa kukosa usahihi wa takwimu za maambukizi ya VVU,” Bi Mahiza aliuambia ujumbe wa TACAIDS uliotembelea ofisini kwake juzi ukiongozwa na mwenyekiti Mtendaji wa tume Dk.Fatma Mrisho
Bi Mahiza akaendelea: Hebu shirikianeni na NBS ili mpate takwimu sahihi za UKIMWI mkoani kwetu…maana siku hizi tunabahatisha.
Hata hivyo, hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete amezindua ripoti mpya ya matokeo muhimu ya utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI na malaria nchini. Utafiti huo ulifanyika kati ya mwaka 2011 na 2012 (THMIS).
Kwa mujibu wa Bi Mahiza, kuna  wajanja wengi wenye asasi zisizo za kiserikali (NGOs) ambao  wanatumia uwepo wa barabara kuu ya Morogoro na vituo vya mizani kuupakazia mkoa wetu kuwa eti maambukizi yanatisha kuliko uhalisia wenyewe. Wanafanya hivyo ili kujipatia hela na misaada kutoka kwa wafadhili wa nje wasiojua ukweli wa mambo na uhalisia wenyewe.
Kwa mfano, Bi Mahiza akaongeza, hivi majuzi tu, kuna kijana wa NGO moja mkoani hapa (siitaji jina), alitoa takwimu eti mkoani Pwani kila siku watu 100 huambukizwa VVU. Haa?! nilishangaa sana. Kwa kuwa na mimi nilikuwa mshiriki katika mkutano huo, nilisimama na kumpinga pale pale.
Huo ni uongo usio kuwa na mfano. Kama  ni kweli, si mkoa mzima wenye watu wasiozidi milioni 1 na laki mbili utakuwa umeambukizwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu?. Ina maana sasa hata mimi mkuu wa mkoa tayari nimeshaambukizwa, akahoji kwa masikitiko.
Kama mkuu wa mkoa, sipendi tabia hii ya kupika takwimu iendelee kwani inakwamisha harakati na mipango yetu dhidi ya UKIMWI
Hata hivyo kiongozi huyo alikiri kuwa kuna baadhi ya maeneo mkoani humo maambukizi ya VVU yalikuwa yanazidi kupanda wakati mengine yalikuwa yanashuka. Alitoa sababu za hali hiyo kuwa ni pamoja na uchumi  katika baaadhi ya familia kuwa mdogo na hulka ya mtu binafsi.
Bado watu wetu wanahitaji elimu kuhusu UKIMWI. Msibweteke na elimu mliyoita mwanzoni. Watu wanapaswa kupewa elimu ya ujasiri katika kupima VVU, elimu ya kuwahudumia wagon jwa, elimu ya kujikinga na maambukizi na elimu ya masula ya lishe na VVU—kusema ukweli bado inahitajika hapa, aliongeza Bi Mahiza
Kwa mujibu wa THMIS 2011-2012, asilimia 5.9 ya wanawake na wanaume kati ya miaka 15 na 49 wana maambukizi ya VVU mkoani Pwani . Hii ni zaidi ya asilimia 0.2 ya kiwango cha maambukizi ya kitaifa (5.7%)
Aidha, kiwango cha maambukizi ya VVU ni kikubwa zaidi maeneo ya mijini kwa wanawake na wanaume kuliko maeneo ya vijijini.
Naye kaimu mganga wa Mkoa Dk. Beatrice Byalugaba alibainisha kuwa baadhi ya wakazi wa Dar es salaam na mikoa mingine jirani wamekuwa wakifuata huduma za tiba za VVU (ARVS) mkoani hapo kwa kuogopa kujulikana mkoani kwao ili kukwepa unyanyapaa.
“Utashangaa wagonjwa wengine wakitoka Dar es salaam kuja kufuata huduma hapa kwetu. Ukiwauliza, wanasema wanaogopa kujulikana makwao,” alisema Dk. Byalugaba akisisitiza ukweli wa kwamba huenda mkoa huo unaonekana kuathirika zaidi kutokana na hali hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tume Dk. Mrisho alitoa wito kwa mkoa kuanza kufikiria jinsi ya kuchangia katika harakati dhidi ya UKIMWI pasipo utegemezi wa wafadhili.
“Ni janga jipya la kitaifa jipya ikiwa hatutakuwa na mbinu zetu wenyewe za kulipia huduma za mapambano dhidi ya UKIMWI. Ni ukweli usiofichika tena kuwa wafadili wanazidi kujitoa na huenda mwakani hali ikawa mbaya zaidi,” alisema Dk. Mrisho aliyekuwa amefuatana katika ziara hiyo na mkuu wa kitengo cha sheria Bi Elizabeth Kaganda
Halmashauri zote nchini zimekuwa zikipata mgao wa fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbai kupitia TACAIDS mara mbili kwa mwaka ili kutoa huduma mbalimbali za masuala ya UKIMWI. Lakini, kutokana na kujitoa kwa wafadahili, halmashauri hizo zitapaswa kujichangisha zenyewe ili huduma zilizokwisha anzishwa ziendelee, “la sivyohili  litakuwa janga jipya la kitaifa,” alibainisha Dk Mrisho