Thursday, May 9, 2013

HABARI NJEMA: Utafiti wa NIMR wa chanjo ya UKIMWI waonyesha matumaini



Dk.Mwinyi
Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imefanya utafiti mpya wa chanjo ya TAMOVAC-01 dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, na matokeo yameonyesha kuwa chanjo hiyo ni salama na ina uwezo mkubwa wa kusisimua mwili na kuzalisha viini kinga katika dozi ndogo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/2014.


Alisema utafiti huo unaendelea kwa washiriki 60 katika Mkoa wa Mbeya.

“Matokeo yalionyesha kuwa chanjo ni salama na ina uwezo mkubwa wa kusisimua mwili na kuzalisha viini kinga katika dozi ndogo,” alisema.

Dk. Mwinyi alisema kuwa taasisi hiyo itaendelea na utafiti wa chanjo inayojulikana kama TAMOVAC-O2,  unaochunguza namna mbalimbali ya utoaji wa dozi ndogo ya chanjo ya Vinasaba vya DNA na MVA ambao utawahusisha washiriki 80 katika mikoa ya Mbeya”.

“Taasisi itaendelea na hatua ya kwanza ya utafiti ujulikanao kama RV262  utakaochunguza aina nyingine ya DNA na MVA dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa lengo la kubaini ubora na usalama wa chanjo hiyo mpya kwa kuchanja washiriki 20 mkoani Mbeya.

Utafiti wa awali uliofanyika nchini kati ya mwaka 2007 hadi 2010, ambao ulijulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 polisi na magereza wa jijini Dar es Salaam, ambao walipewa chanjo hiyo na baadaye kuachwa wakiishi maisha yao ya kawaida kwa muda wa miaka mitano.

Gazeti linalochapishwa kila siku (siyo) NIPASHE, liliwahi kumnukuu,  Profesa Muhammad Bakari, aliyeongoza jopo la madaktari waliofanya utafiti huo akisema kuwa utafiti huo umezaa matunda.

Alisema  utafiti huo ulithibitisha kwamba chanjo ya DNA –MVA waliyopewa askari hao, ilikuwa salama na yenye uwezo wa kufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).  Utafiti huo ulifanyika nchini kati ya mwaka 2007-2010 na 2008-2012.

“Chanjo hiyo inaweza kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU kwa asilimia 100 kwa washiriki waliopatiwa chanjo zote tano. Haya ni matokeo mazuri sana kupita hata matarajio  ya watafiti, pia ni ya muhimu katika harakati za kutafuta chanjo dhidi ya VVU,” alinukuliwa.

Bila kutaja sababu za kusitisha utafiti huo, Dk. Mwinyi alisema utafiti huo ulisitishwa na kwamba hakuna madhara watakayopata binadamu kwa kuwa hakuna aliyechanjwa.

Wakati huo huo, Dk. Mwinyi alisema Wizara imekamilisha maandalizi ya awali ya kutoa chanjo ya Human Papilloma Virus kwa wasichana waliofikia umri wa kubalehe kwa ajili ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.

“Utoaji wa chanjo hiyo utaanza katika Mkoa wa Kilimanjaro ,” alisema na kufafanua kuwa wizara yake itaanzisha chanjo ya pili ya surua ili kutoa kinga dhidi ya ugonjwa huo. Chanjo hiyo itatolewa kwa watoto wenye umri wa miezi 18.

Dk. Mwinyi alisema Mamlaka ya Chakula na Dawa, (TFDA), ilikusanya jumla ya taarifa 160 na madhara ya tokanayo na matumizi ya dawa za ALU zilikusanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita na hivyo kufikisha taarifa 8,000 zilizokusanywa.

Alisema katika mwaka huu wa fedha Mfuko wa Bima ya Afya,  utahakikisha kuwa huduma za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), zinaanza kupatikana hadi ngazi ya hospitali za rufaa kwa kuanza na Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Ruvuma, Pwani, Tanga, Lindi na Kilimanjaro na zitasimamiwa na ofisi za Mfuko za Mikoa.

Pia alisema utasajili kliniki za magonjwa maalum zikiwamo kliniki za watoto, mifumo ya mikojo, magonjwa ya akinamama na moyo.

0 comments:

Post a Comment