Friday, April 26, 2013

TACAIDS yakutana na wahariri wakuu—yawataka kupeleka ujumbe sahihi na haraka dhidi ya UKIMWI



Jopo la wakuu wa TACAIDS
Katikati ya wiki hii viongozi wakuu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) walikutana na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari na kuwataka kubeba jukumu la kuupasha umma kuhusu madhara ya VVU na jinsi ya kuendelea kujilinda ili kufikia azma ya maambukizo “sifuri” vifo “sifuri” na unyanyapaa “sifuri”.


Wakiongozwa na Mwenyikiti Mtendaji wa TACAIDS Dk. Fatma Mrisho, viongozi hao waliwataka wana-habari hao kutumia uzoefu, ueledi na taaluma yao katika kusaidia jukumu la kitaifa la kutokome za maambuki zo ya VVU na UKIMWI kwa jamii ya kiTanzania kwa kupeleka taarifa sahihi.


Katika mkutano huo, Dk. Mrisho alifuatana na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Dk. Raphael Kalinga, Mkurugenzi wa Fedha Bi Beng Issa, Mkurugenzi wa Ulaghibishi na Habari Bw. Jumanne Issango, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Utathimini (M&E) Dk. Jerome Kamwera


Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Mwitikio wa Kitaifa Bw.Sebastian Kitiku, Meneja Mawasiliano Bi. Gloria Mziray, Mwanasheria wa Tume Bi. Elizabeth Kaganda na Afisa Ulaghibishi Bw. Simon Keraryo
Sehemu ya wahariri wakichukua dondoo


Katika kile kinachoonekana kuwa Tume imedhamiria kuufikia umma kupitia vyombo vya habari wakuu wa tume hiyo walifungua milango kwa wahariri hao kwa kuwakaribisha kutembelea makao makuu mapya ya taasisi hiyo nyeti ili wapate takwimu, taarifa na ufafanuzi wowote ule utakaosaidia jamii kujihami na kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.


Makao mapya ya TACAIDS yako mtaa wa Lithuli mkabala kabisa na ofisi za WAMA—Wanawake na Maendeleo.


“Tunawakaribisha ofisini kwetu kupata ufafanuzi wowote kuhusu jambo lolote au taarifa zozote ambazo mnadhani zitawawezesha kupeleka ujumbe sahihi kwa wananchi—lengo letu sote ni kuhakikisha tunakomesha maambukizo mapya ya VVU miongoni mwa umma wa kiTanzania, akasema Dk. Mrisho


Na kuongeza “kama mtaona shida au taabu kufika ofisini kwetu, basi tumieni mawasiliano ya kisasa—email kwa anwani hii: ec@tacaids.go.tz


Mwanasheria wa tume Bi.Kaganda akifafanua jambo
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao walibainisha badhi ya mafanaikio ya kujivunia kwa tume hiyo kuwa ni pamoja na kupungua kwa maambukizo mapya kutoka asilimia 14 (14%) hadi asilimia 5.1(5.1%) kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI ya 2011 na 2012 iliyozinduliwa hivi karibuni.


Mafanikio mengine ni ushiriki wa wadau wengi katika vita dhidi ya VVU, kuongezeka kwa raslimali fedha, kutambua njia za maambukiz0, kuwa na sheria ya UKIMWI, kuwa na mikakati ya kuongoza mapambano, kupanuka kwa huduma za UKIMWI, kuanzisha huduma za tiba na matunzo na kuanzishwa kwa mifumo ya uratibu.


Kuhusu changamoto zinazoikabili tume hiyo ni pamoja na kutokufuatiliwa kikamilifu kwa sera na mikakati ya kitaifa dhidi ya UKIMWI, unyanyapaa na kutengwa kwa WAVIU, uhaba wa kifedha katika kutekeleza mwitikio wa kitaifa na wakati mwingine ukosefu wa uwajibikaji kwa baadhi ya wadau.
Wahariri wakipewa taarifa na TACAIDS

Baadhi ya wahariri waliokuwepo ni kutoka vyombo vya The Guardian Limited, ITV na Radio One, Habari Leo, Mwananchi, New Habari Corporation, Changamoto, Morning Star Radio FM, Radi, Hoja, Majira, Daily News na  Praise Power Radio FM.

0 comments:

Post a Comment