WAJUMBE wa kamati ya kudumu ya
bunge ya katiba,sheria na utawala wametaka kupewa umuhimu wa kutembelea mara
kwa mara miradi na shughuli mbali mbali zinazohusiana na kampeni dhidi ya UKIMWI nchini ili kujua hasa
thamani ya fedha (value of money) zinazotolewa na serikali pamoja na wadau
mbalimbali wa maendeleo katika kupambana na ugonjwa huo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mh. Chana Pinda, wajumbe hao
walitoa dai hilo jijini jana walipokutana na viongozi wa ngazi za juu wa
Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS).
“Hatuwezi kuhakiki thamani ya fedha zinazoelekezwa katika
miradi ya kupambana na UKIMWI kama tutaendelea kuletewa ripoti na taarifa
kwenye makaratasi tu. Tunapaswa kufika kwenye maeneo ya miradi ili kuona
walengwa wananufaikaje,” alisema Mh Deogratius Ntukamazina, Mbunge wa Ngara na
kiongozi mstaafu katika tume ya utumishi.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mh.Abbasi Mtemvu, mbunge wa
Temeke ambaye alisema ikiwa kamati itaendelea kutengwa katika shughuli muhimu zinazohusiana
na kampeni dhidi ya UKIMWI, ni dhahiri itaendelea kupitisha bajeti ambayo
huenda haiwanufashi walengwa.
Kama kamati haiwezi kufika huko kwenye miradi au halmashauri zinazopelekewa
mamilioni ya pesa ili kupambana na UKIMWI kila mwaka, ni dhahiri kwamba kamati itakuwa
inapitisha pesa ambazo haijui mwisho wa siku zinafanya nini, alisema Mh Mtemvu
Akisisitiza umuhimu huo, Mwenyekiti Mh. Chana Pinda alisema ziara
kama hizo zitaiwezesha kamati yake kujua kinachoendelea huko kwenye jamii.
“Wajumbe wanataka ziara hizi sio kwa ajili ya posho, bali kwa
ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya UKIMWI nchini na hivyo basi kuweza
kujua kinachoendelea huko mashinani na kuchukua hatua stahiki,” alisema
Mh.Pinda
Wajumbe hao walitoa dai hilo mara baada ya naibu mwenyekiti
wa TACAIDS Bi Beng’ Issa kutoa taarifa ya mwenendo wa kampeni dhidi ya UKIMWI
nchini. TACAIDS ndiyo mratibu wa shughuli zote a UKIMWI nchini ikifanya kazi
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu
Katika taarifa yake, Bi Issa alisema kuwa licha ya kukabiliwa na ufinyu wa bajeti
unaochangiwa na kupungua kwa misaada ya wahisani, serikali ilikuwa imejipanga
kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI (VVU) kwenye jamii ya kitanzania
kwa silimia 9
Ili kufikia lengo hilo pamoja na mengine, serikali ilikuwa
inajipanga kuhakikisha mfuko wa UKIMWI (AIDS Trust Fund) ambao ni jitihada za
watanzania wenyewe unaanza kufanya kazi vizuri.
Takribani shilingi bilioni 300 zitakuwa zinakusanywa kutoka
serikalini kupitia mfuko huo kila mwaka.
Aidha mikakati mingine ya kufikia azma hiyo ni kuhakikisha
mamlaka za serikali za mitaa zinatenga fedha kutoka kwenye vyanzo vyake kwa
ajili ya shughuli za UKIMWI.
“Aidha tumejipanga kuanza kufanya ukaguzi wa matumizi ya
fedha za UKIMWI kwenye mamlaka za serikali za mitaa kuangalia matumizi kwa
thamani ya fedha,” alisema Bi Issa ambaye pia ni Mkurugenzi wa masuala ya fedha
wa TACAIDS.
Wakati huo huo, Kamati hiyo ya bunge iliitaka TACAIDS
kuharakisha kutoa utafiti mpya wa masuala ya UKIMWI nchini ili kuwa na takwimu
mpya na sahihi kuhusu ugonjwa huo. Hadi jana, takwimu zinazotumika ni zile za
utafiti wa hali ya UKIMWI nchini uliofanyika mwaka 2007 na 2008 ulioonyesha
kiwango cha maambukizi cha asilimia 5.7
Akijibu rai hiyo, Bi Issa alisema tume ilikuwa inajiandaa
kutoa takwimu mpya za hali ya UKIMWI nchini katika kipindi cha miezi miwili
ijayo mara baada ya kukamilika kwa utafiti mpya uliofanywa na Shirika la Takwimu
la Taifa (TBS)