Sunday, November 18, 2012

Jilinde VVU kwanza kabla hujafikiria Taifa- Dk.Kalinga


MKURUGENZI wa sera na mipango katika Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dk. Raphael Kalinga amerejea wito wake kwa jamii kwamba mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI yaanze kwa mtu binafsi. 

Dk. Kalinga (watatu kulia waliosimama)
Kwa kutambua hilo, mtu binafsi ataweka mikakati thabiti ya kujilindi yeye binafsi hata kabla ya kumfikiria mwenza wake, familia yake na hatimae taifa lake.

Dk. Kalinga alitoa msimamo wake huo ambao amekuwa akiusisitiza katika siku za hivi karibuni wakati alipozungumza na mtandao wa blog ya Zuia UKIMWI Tanzania.

“Napenda nieleweke vizuri. Ninaposema kuwa tatizo la UKIMWI ni la mtu binafsi kwanza kabla halijawa la kitaifa, nina maana kwamba taifa haliwezi kuwepo kama hakuna mtu binafsi. Mtu binafsi anaungana na mwenza kutengezeza familia, familia inatengeneza jamii, baadae  kijiji, tarafa, wilaya, mkoa na hatimae taifa,” akasema Dk.Kalinga.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kama sehemu ya kutimiza ndoto ya kitaifa ya kutokomeza kabisa kabisa kwa kiwango cha “0”  maambukizo mapya ya VVU, unyanyapaa pamoja na vifo vinavyotokana na VVU/UKIMWI ifikapo 2015, kila mwananchi kwa nafasi yake anapaswa kujilinda kwanza na kuhakikisha hapati maambukizo yoyote.

Na kwa yule aliyekwisha ambukizwa azingatie masharti ya kinga na tiba ambayo yatamfanya aendelee kuwa mwenye siha lakini pia pasipo kupata maambukizo mengine mapya (re-infection) 

Dk. Kalinga akaongeza kuwa, kwa mtu anayemsikia haraka haraka, anaweza kuhisi kuwa anapingana na tamko la serikali la mwaka 2005 (enzi za utawala wa Rais Mstaafu Benjamini W Mkapa) lililoutangaza UKIMWI kuwa janga la kitaifa. 

Tangu kipindi hicho, serilai kwa kushirikiana na wadao mbali mbali katika mapambano hayo ilichukua hatua muhimu na imara kupambana na maambukizo na kuzidi kusambaa kwa VVU na UKIMWI miongoni mwa jamii ya Tanzania.

Mojawapo ya mafanikio yab hivi karibuni ni kupungua kwa kiwango cha maambukizi miongoni mwa watanzania kutoka 7.2% hadi 5.7% kwa mujibu wa takwimu za taifa za 2008/2009. 

Njia zinazotumika kupunguza maambukizi zimekuwa tofauti lakini mojawapo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma ya kujinga na maambukizo ya VVU , kutoa dawa kwa mama wajawazito wenye VVU ili kuzuia wasiwaambukize watoto wanaotarajia kuwazaa, kuanzisha tiba (ARVs) kwa watu wanaoishi na VVU pamoja na kampeni za kutahiri wanaume wasiotahiriwa

Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, bado baadhi ya wananchi wameendelea kushabikia au kutekeleza tabia ambazo zinapelekea maambukizo mapya. Mfano mzuri ni ule wa watu kuendekeza tabia au mila za kuwa na wenza (wapenzi) wengi, maarufu kama mtandao wa ngono.

0 comments:

Post a Comment